Tuesday, 3 November 2015

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Izia, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa na wanafunzi wa darasa la tatu wakitoka kukagua uharibifu wa darasa moja la shule hiyo baada ya paa lake kuezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua juzi. (Picha na Peti Siyame).

MVUA kubwa imenyesha katika mikoa ya Rukwa na Mwanza, na kusababisha maafa, ikiwemo vifo vya watu wawili na familia kadhaa kukosa makazi kutokana na nyumba kubomoka.
Aidha, mvua hizo zimesababisha kufungwa kwa muda uwanja wa ndege wa Mwanza kutokana na kujaa maji.
Wakati jijini Mwanza, watu wawili wamepoteza maisha kutokana na kusombwa na maji ya mvua iliyonyesha jana, kwa upande wa mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa, familia 20 hazina mahali pa kuishi kutokana na nyumba zao kubomoka na nyingine kujaa maji kutokana na mvua zilizonyesha juzi.
Mvua hizo zinasadikiwa ndiyo mwanzo wa El-Nino kutokana na taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kueleza jana kwamba, kutakuwa na mvua za El-Nino, kama ilivyokuwa imeelezwa katika taarifa yake ya Septemba mwaka huu.
Vifo, miundombinu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo katika mkutano wake na waandishi wa habari, alisema mmoja wa waliopoteza maisha, ni mwendesha bodaboda wa Kirumba aliyekuwa amepakiza wanafunzi wawili akiwapeleka shuleni.
Kuhusu wanafunzi hao, Kamanda alisema, taarifa zake hazijathibitishwa kama pia wao wamepoteza maisha, ingawa tukio hilo limo katika orodha ya athari za mvua hizo. Alisema mtu mwingine alionekana akiwa anaelea katika maji eneo la Mabatini, lakini baadaye mwili wake haukuonekana kutokana na mafuriko hayo.
“Tumepokea taarifa juu ya mvua hizi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza na tunaendelea kukusanya taarifa na kuchukua hatua stahiki,” alisema Kamanda Mkumbo.
Kuhusu uwanja wa ndege, mvua hizo zilisababisha kufungwa kwa saa tano kwa uwanja wa ndege wa Mwanza baada ya kujaa maji. Meneja wa uwanja wa Ndege wa Mwanza, Esther Madale alimwambia mwandishi wa habari hizi kwamba uwanja huo ulilazimika kufungwa kwa saa tano kwa ajili ya kuwezesha wahandisi, kufanya uchunguzi wa miundombinu yake.
Hakuna ndege iliyoruhusiwa kutua katika muda huo. “Ni kweli tulikumbwa na mkasa huo wa mvua ambazo zilinyesha mfululizo na kusababisha kufungwa kwa uwanja kwa muda…kwa sasa tunavyoongea tayari huduma zimerejea katika hali yake ya kawaida,” alisema Madale.
Uwanja huo wa ndege upo katika matengenezo makubwa, ikiwamo mnara wa kuongozea ndege, njia za kurukia ndege ambazo sasa ni meta 2000 na zinaongezwa hadi kufikia meta 3300. Ukarabati huo ulianza mwaka 2012 na ulitarajiwa kumalizika Oktoba mwaka huu.
Wakosa makazi
Kwa upande wa Rukwa, mvua ya mawe iliyonyesha juzi mjini Sumbawanga, iliambatana na upepo mkali ambao ulisababisha zaidi ya familia 20 kukosa makazi ya kudumu. Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Manispaa ya Sumbawanga, George Lupilya alisema Kamati ya Maafa inaendelea kutathmini uharibifu uliosababishwa na mvua hiyo.
Mvua hiyo iliyonyesha kwa takribani saa moja, imewaathiri pia wafanyabishara wa nafaka katika Soko Kuu la Mandela mjini hapa kwa kuwasababisha hasara inayokadiriwa kufikia zaidi ya Sh milioni 30.
Mvua hiyo iliezua mapaa ya madarasa mawili na choo katika Shule ya Msingi Izia, yenye idadi ya wanafunzi wapatao 984. Pia iliangusha miti , nyaya za umeme na kuharibu miundombinu ya barabara .
Akizungumza na gazeti hili, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Izia, Antoni Simon alisema ni bahati kwamba mvua ilinyesha Jumapili, siku ambayo wanafunzi wanakuwa mapumziko vinginevyo ingeweza kusababisha maafa makubwa kwa binadamu.
Aidha, uzio wa shule maalumu ya watoto wasioona na wenye uono hafifu iliyoko eneo la Malangali, Manispaa ya Sumbawanga, umeanguka na vyumba vya ofisi na madarasa kujaa maji.
Mwenyekiti wa Soko Kuu la Mandela, Zalubabeli Luvanda alisema vyumba vya biashara vilivyokuwa vimehifadhi nafaka, yakiwemo mahindi , maharage na vitunguu, vilijaa maji na kusababisha hasara ya Sh 33, 270, 000.
Mmoja wa wamiliki wa vyumba hivyo , Msulwa Msepuka, alisema magunia 300 ya mahindi yameharibiwa na maji na kupata hasara ya takribani Sh milioni 15.
Mwathirika mwingine wa mvua hizo, ni mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Mama Njema ambaye kwa mujibu wake, magunia 11 yaliyojaa vitungu yamelowa. Mwandishi wa habari hizi aliyefika sokoni hapo, alishuhudia madimbwi ya maji .
El-Nino imeanza
Katika taarifa ya TMA kwa vyombo vya habari jana, ilisema kuendelea kuongezeka kwa joto katika maeneo ya Bahari ya Pasifiki kunaonesha kuimarika kwa mvua za El-Nino kama ilivyoelezwa katika taarifa iliyotolewa Septemba, mwaka huu.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, imesema mvua zimeshaanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini hususani Ukanda wa Ziwa Viktoria, Kanda ya Magharibi na Nyanda za Juu, Kaskazini Mashariki na zinataraji kuwa za juu ya wastani.
“Hata hivyo, mifumo mingine ya hali ya hewa ikiwemo mwitikio wa mfumo ya hali ya hewa katika Bahari ya Hindi imekuwa na mchango hasi kinyume na ilivyotarajiwa katika mwenendo wa mvua za Vuli nchini katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2015 na kusababisha vipindi virefu vya upungufu wa mvua katika mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.chanzo habarileo

0 comments:

Post a Comment

wanaotutazama


hit counter

tz shiling exchange

MY CALENDAR

Total Pageviews

Recent Posts

find us on twitter

Find Us On Facebook

MATANGAZO