Thursday, 26 November 2015


Rais John Magufuli amesitisha maadhimisho ya siku ya UKIMWI kitaifa ambayo yalikuwa yafunguliwe mkoani Singida leo na kufikia kilele chake Desemba mosi mwaka huu mjini humo.
Badala yake Rais Dk Magufuli ameagiza fedha zote ambazo zilitengwa na serikali pamoja na wahisani mbalimbali kwa ajili ya maadhimisho hayo zielekezwe kununua vifaa tiba na vitendanishi.
Ofisa Habari Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Nadhifa Omar, alisema Rais ametoa agizo hilo leo wakati maandalizi kwa ajili ya ufunguzi wa maonesho yaliyoanza Novemba 24 yakiendelea.
“Rais ameagiza kusitisha maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya UKIMWI duniani ambapo kitaifa yalikuwa yafanyike Desemba mosi, mwaka huu mjini Singida na kutaka fedha za maandalizi zielekezwe katika manunuzi ya vifaa tiba kwa ajili ya hospitali nchini,”alisema Omary.
Omary alisema serikali ilitenga kiasi cha shilingi milioni 18 kwa ajili ya maadhimisho hayo huku kila mshiriki katika maonesho hayo akichangia kiasi cha shilingi laki tano.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Dk Fatma Mrisho alisema maadhimisho ya mwaka huu yakuwa yatanguliwe na maonesho ya wadau yatakayojumuisha huduma mbalimbali zikiwamo za utoaji elimu na burudani.
Dk Mrisho alisema huduma nyingine zilizopangwa kutolewa katika maadhimisho hayo ya wiki moja ni upimaji wa hiari wa watu zaidi ya 3,500 wanaoishi na virusi vya Ukimwi na utoaji ushauri nasaha, upimaji wa shingo ya uzazi, sukari, uzito, damu na kupata elimu itakayotolewa kupitia vikundi vya sanaa na burudani.
Maadhimisho ya mwaka huu yanachagizwa na kaulimbiu ya ‘Tanzania bila maambukizi mapya ya VVU, vifo vitokanavyo na UKIMWI na ubaguzi na unyanyapaa inazewekana.’
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni kuwa maadhimisho hayo yanatarajiwa kuanza Novemba 24 mwaka huu kwenye viwanja vya Peoples Club ambapo uzinduzi utakuwa Novemba 25 kabla ya kilele, Desemba mosi.
Hii ni mara ya tatu tangu Rais Dk Magufuli aingie madarakani kuzuia maadhimisho yanayogharimu fedha nyingi na sherehe na fedha zake kuelekeza ikanunulie vifaa tiba mahospitalini.
Awali Rais aliagiza fedha zilizotengwa kwaajili ya hafla ya uzinduzi wa Bunge zaidi ya shilingi Milioni 225 ziende kununulia vitanda vya hospitali ya taifa Muhimbili.
Aidha Rais pia alisitisha maadhimisho ya siku ya Uhuru Desemba tisa mwaka huu na badala yake watu wafanye kazi katika maeneo yao ya kazi hasa usafi wa mazingira.

0 comments:

Post a Comment

wanaotutazama


hit counter

tz shiling exchange

MY CALENDAR

Total Pageviews

Recent Posts

find us on twitter

Find Us On Facebook

MATANGAZO