Tuesday, 10 November 2015
09:59
Unknown
No comments
RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), amekutana katika Ikulu ya Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF) katika Uchaguzi Mkuu uliofutwa.
Taarifa za uhakika zilizopatikana hapa zimesema kwamba viongozi hao walikutana kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi ulioacha utata visiwani chini ya mazungumzo yaliyohudhuriwa na viongozi wakuu wastaafu ambao ni wazee wanaoheshimika.
Ikulu ya Zanzibar haikuwa tayari kusema lolote kuhusu mazungumzo hayo ambayo yamekuwa yakisubiriwa kwa hamu na wananchi wa Zanzibar kwa lengo la kujua mustakabali wa kisiasa na kumaliza joto la kisiasa lililodumu mara baada ya wananchi kupiga kura Oktoba 25, mwaka huu na baadaye kufutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Ofisa mmoja wa Ikulu ya Zanzibar, alithibitisha na kukiri kuwepo kwa mazungumzo hayo baada ya kuuona msafara wa Makamu wa Kwanza wa Rais ukiingia Ikulu, lakini hakuwa tayari kufafanua zaidi.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia kwa Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi ilieleza kuwa itawachukulia hatua wote waliovuruga uchaguzi huo, huku CUF wakilalamika na kupinga maamuzi ya ZEC.
Kuanzia hapo hali ya joto la kisiasa limepanda huku wananchi wakisubiri kwa hamu kujua mustakabali wa ufumbuzi wa tatizo hilo la kufutwa kwa uchaguzi. Katika hatua nyingine, wagombea 27 wa uwakilishi kupitia CUF walioshinda katika majimbo yao kwenye uchaguzi huo wamesema ushindi wao uliotangazwa na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo hauwezi kubatilishwa na ZEC.
Wawakilishi hao ambao jana walizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam na kuonesha hati za ushindi ambazo walikabidhiwa na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo yao, walisema chombo pekee chenye mamlaka ya kutengua matokeo hayo ni Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Katika msimamo wao wa pamoja walimtaka Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kutengua tamko lake waliloliita ni batili la kufuta uchaguzi wa Zanzibar na badala yake wakataka tume hiyo ikamilishe taratibu za majumuisho ya kura za urais wa Zanzibar ili hatimaye Rais atangazwe na aitishe baraza jipya la wawakilishi.
Wawakilishi hao walisema walipewa hati hizo za ushindi baada ya wasimamizi wa majimbo kuridhika kuwa hatua zote za uchaguzi zilikwenda vizuri na hakukuwa na kasoro yoyote. Katika madai yao walisema idadi ya watu waliopiga kura katika kila kituo ni pungufu ya watu 350 ambayo ilitakiwa katika kila kituo.
Akizungumza kwa niaba ya wawakilishi hao, Abubakar Khamis Bakary alisema Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar imetoa uwezo na mamlaka yote ya kusimamia na kuendesha uchaguzi wa wawakilishi na madiwani kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo.
Bakary aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, alisema hakuna sehemu yoyote katika Katiba ya Zanzibar wala katika sheria ya uchaguzi inayotoa uwezo kwa Mwenyekiti wa Tume au ZEC kufuta uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi katika kufanya kazi yake ya kusimamia na kuendesha uchaguzi wa wawakilishi na madiwani.chanzo habari leo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


0 comments:
Post a Comment