Thursday, 22 October 2015

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene akifafanua jambo wakati wa mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari Dar es Salaam jana. Kulia ni msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Advera Bulimba. (Picha na Mroki Mroki).

JESHI la Polisi nchini limewaondolea hofu wananchi juu ya kuwepo kwa vurugu na vitendo vya uvunjifu wa amani siku ya Uchaguzi Mkuu Jumapili wiki hii; na kuonya kuwa yeyote aliyejipanga kuvuruga uchaguzi, atadhibitiwa.
Akizungumza katika mkutano wa Idara ya Habari (MAELEZO) na wahariri wa vyombo vya habari Tanzania, Dar es Salaam jana, msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alisema jeshi hilo limejipanga vyema kuhakikisha uchaguzi utakuwa huru na wa haki pasipo kuwepo na vurugu nchini.
“Polisi tumejiandaa kutumia weledi katika utendaji kazi siku ya uchaguzi kwa kufuata taratibu na sheria zetu za kazi na tunawahahakishia wananchi wote kuwa wajitokeze kwa wingi kupiga kura na wala wasiwe na hofu juu ya amani,” alisema Bulimba.
Alisema wananchi waondoe hofu juu ya polisi, kwani itatenda haki na halitamuonea mtu yeyote, kama ambavyo inadhaniwa huku ikitoa tahadhari kwa waliojipanga kuvuruga uchaguzi ama katika utangazaji matokeo.
Bulimba alisema Polisi imejipanga kudhibiti viashiria vyote vya amani na utulivu uliopo nchini huku ikiwaomba wananchi kuhakikisha siasa haivuki kuwa jinai. “Kazi yetu ni sawa na kung’ata na kupuliza, mtu yeyote ambaye atafuata taratibu, hatuna shida naye, lakini yule ambaye atakiuka taratibu, sheria na kanuni, huyo tutamdhibiti…hapo ndio kung’ata na kupuliza,” alieleza.
Chikawe apiga marufuku mikusanyiko Aidha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alisema sheria za nchi zinatakiwa kufuatwa siku ya uchaguzi, ikiwamo kutoruhusiwa kuwapo kwa mikusanyiko na maandamano yasiyokuwa ya kihalali.
Chikawe aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Jeshi la Polisi limetakiwa kutimiza wajibu wao, wafanye kazi bila kuonea mtu yeyote na wala kumuogopa yeyote. “Sheria ya uchaguzi inasema watu wapige kura saa moja hadi saa 10 na baada ya hapo wanaweza kusogea zaidi ya meta 200 na sio kituoni, lakini pia zipo sheria za nchi zinazohusu mikusanyiko na maandamano ambazo hazitofutwa kwa sababu ya uchaguzi,” alisema Chikawe.
Alisema suala kubwa ni kuzingatiwa kwa amani, wananchi wazingatie sheria. Alisema kama lipo kundi, ambalo litahitaji kuandamana ama kukusanyika, linapaswa kuomba kibali kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Polisi akiwaambia raia muondoke mahali fulani ni vyema kutii na kutimiza ili kwamba wasije wakachukua hatua nyingine ambayo inaweza kutafsiriwa vinginevyo,” alisema Chikawe na kuongeza kuwa kutumia nguvu za kupita kiasi kunatokana na kutokutii kwa raia.
Mwambene aonya waandishi Awali, akizungumza na wahariri hao, Mkurugenzi wa Maelezo, Assah Mwambene aliviasa vyombo vya habari kufanya kazi yake ya kuhabarisha umma kwa kufuata misingi ya taaluma hiyo, lakini kubwa zaidi kuweka uzalendo na maslahi ya nchi mbele.
“Vyombo vya habari ni mhimili wa nne wa dola, vina wajibu wa mpana kuliko mihimili mingine yoyote katika kuimarisha demokrasia, amani na utulivu katika taifa lolote,” alisema Mwambene.
“Kuna viashiria vingi vya uvunjifu wa amani, sisi kama vyombo vya habari tunapaswa kuviangalia kwa mapana, ili kudumisha amani, lakini tukihabarisha umma kwa kufuata sheria na miongozo ya uandishi,” alisema Mwambene.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kupitia Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utangazaji, Frederick Ntobi imeonya waandishi wa habari kutojiingiza katika ushabiki na kuingilia kazi za taasisi nyingine katika uchaguzi.
Akizungumza kwa niaba ya wahariri wenzake, Wallace Mauggo kutoka The Guardian Ltd, alisema kila Mtanzania ahakikishe uchaguzi unafanyika na kufanikiwa na yeyote atakayekiuka sheria, basi achukuliwe hatua zinazostahiki.
Bana aisifia NEC Wakati huo huo, wanasiasa wametakiwa kuacha kuzusha maneno na kutoa visingizio vinavyoashiria uchaguzi hautofanyika kwa uhuru na haki, jambo linaloweza kusababisha hofu ya matokeo kipindi na baada ya uchaguzi.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Siasa cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana, wakati akijibu swali kuhusu utendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwenye uzinduzi wa Kituo cha Uangalizi wa Uchaguzi Tanzania, uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Alionesha kuwashangaa baadhi ya wanasiasa wanaozusha hofu hizo, zinazoashiria kutoiamini tume hiyo, wakati tume hiyo ilipowateua kuwa wagombea waliiamini. Alisema kumekuwa na baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakilalamikia tume hiyo na kuonesha wasiwasi kuwa huenda isifanye haki katika uchaguzi, wakati ni tume hiyo hiyo ndio waliyoitumia katika michakato yote ya uchaguzi, kuanzia uandikishwaji hadi kwenye uteuzi wa majina ya wagombea.
“Nawaomba wanasiasa tuachane na visingizio na malalamiko yasiyo na lazima, tuingie kwenye uchaguzi bila kuamini kuwa uchaguzi hautafanyika kwa uhuru, hii tume mnayoilalamikia ilipoteua majina yenu hamkulalamika kuwa si huru, sasa iweje kwenye matokea isiwe huru,” alisisitiza.
Alisema kwa hali ilivyo, ni dhahiri kuwa chaguzi za Tanzania zimekuwa zikibadilika kadri miaka inavyokwenda ambapo ukilinganisha na uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995, kwa sasa chaguzi zimeimarika na kufanyika kwa uwazi mkubwa.
Alisema hali hiyo, inatokana na utendaji mzuri wa Tume ya taifa ambayo imesheheni wajumbe wa kuaminika na ni tume inayofanya vizuri kuliko tume zote za uchaguzi zilizopo katika nchi za Jangwa la Sahara.
Alisema anashangazwa na madai ya baadhi ya wanasiasa wanaonesha wasiwasi wa uchaguzi kuchafuliwa, wakati tume hiyo, kati ya wajumbe iliyonao ni pamoja na majaji wazito watano ambao si rahisi kuhoji utendaji wao.
“Katika Jangwa la Sahara tume yetu ni the best, hivi kweli ni nani anayeweza kuhoji integrity ya majaji hawa watano waliopo katika tume? Kama utahoji utendaji wao basi huo utakuwa ni upungufu mkubwa,” alisema Dk Bana.chanzo habarileo

0 comments:

Post a Comment

wanaotutazama


hit counter

tz shiling exchange

MY CALENDAR

Total Pageviews

Recent Posts

find us on twitter

Find Us On Facebook

MATANGAZO