MGOMBEA Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli amekanusha kauli ya mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa kwamba fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Tanga, zimehamishiwa katika Bandari ya Bagamoyo.
Amesema kauli hiyo iliyotolewa na Lowassa juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara mjini Tanga ni ya uchochezi dhidi ya Watanzania na kwamba adhabu ya mgombea huyo ni kupigiwa kura ya Hapana katika uchaguzi wa keshokutwa.
Katika hatua nyingine, Dk Magufuli amebainisha kuwa baada ya kazi kubwa ya ujenzi wa shule za sekondari za kata, iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, ameamua serikali yake kupeleka nguvu katika kuboresha elimu inayotolewa katika shule hizo.
Pia, alisema serikali yake itapaisha mishahara ya walimu, kuwajengea nyumba za kisasa na kuboresha maisha ya wafanyakazi wengine. Aliyasema hayo akiwa katika ziara ya kutembelea majimbo mbalimbali ya uchaguzi katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020 na kuomba kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano.
Alitembelea majimbo ya Kibamba, Chalinze, Kibaha Vijijini, Kibaha Mjini na Kawe katika eneo la Bunju. Kumhusu Lowassa Akieleza kwa masikitiko, Dk Magufuli alisema kauli ya Lowassa kwamba Serikali imehamisha fedha zilizotengwa kwa ujenzi wa Bandari ya Tanga zimehamishiwa katika ujenzi wa Bandari ya Mbegani mjini Bagamoyo ni kauli ya uchochezi na inayopaswa kulaaniwa na Watanzania wote, kwa vile imelenga kuwagawa wananchi.
Alisema serikali inayo mipango ya kujenga Bandari za Tanga, Bagamoyo, Mtwara, Mwanza na nyinginezo kwa kutenga fedha za kujenga kila bandari na si sahihi kwamba fedha za Tanga zimehamishiwa Bagamoyo.
“Kauli hii inadhihirisha ubaguzi wa wazi kabisa aliokusudia kuufanya mgombea huyu dhidi yenu watu wa Chalinze na Bagamoyo na dawa pekee ya mtu kama huyu ni kumnyima kura na kunipatia mimi,” alisema Dk Magufuli.
Alifafanua kuwa Bandari ya Bagamoyo, inajengwa chini ya uwekezaji wa Ushirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP). Aidha, alisema pamoja na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo huko Mbegani, aliyosema itajengwa na mwekezaji kutoka nchi za Falme za Kiarabu (UAE), pia katika eneo hilo limetengwa eneo maalumu la kujenga viwanda, ambapo zaidi ya viwanda 1,000 vitajengwa na kuchochea ajira kwa Watanzania na pia kuchangia ukuaji wa uchumi.
“Nataka niwahakikishie watu wa Tanga kwamba mpango wa kuijenga Bandari ya Tanga upo pale pale na nitaijenga bandari hiyo mapema sana nikiingia madarakani. Lakini si bandari hiyo tu, pia tutajenga bandari nyingine za Mtwara, Lindi na Mwanza,” alisema.
Akizungumza katika mkutano wa Kibamba, Dk Magufuli aliahidi kuelekeza nguvu nyingi katika kuboresha elimu kwenye shule za sekondari za kata, baada ya awamu iliyomtangulia ya Rais Kikwete kupata mafanikio makubwa ya ujenzi wa shule hizo kwa kiwango kikubwa.
Alisema baada ya uboreshaji wa elimu nchini, pia atashughulikia mishahara ya walimu ili kuifanya kupaa kwa kiwango kikubwa na kuwajengea nyumba za kisasa na kuwalipa malimbikizo yote ya posho, huku akisema mpango huo utawahusu pia wafanyakazi wa sekta nyingine.
Katika mkutano wa Kibaha, kama alivyowaahidi wakazi wa Chalinze, aliwaahidi pia wakazi wa Kibaha kuboresha miji hiyo kwa kiwango kikubwa kutokana na kuwepo kwa ujenzi wa barabara za kisasa za njia sita, kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze, hatua itakayokuza uchumi.
Alizungumzia mikakati ya serikali kutumia gesi iliyopatikana katika eneo la Ruvu wilayani Bagamoyo katika kuharakisha mpango wa serikali yake kuwa serikali ya viwanda na hivyo kuchochea ukuaji wa mapato ya serikali na wananchi mmoja mmoja.chanzo habari leo

0 comments:
Post a Comment