MWENYEKITI wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amemfananisha mgombea
urais wa chama hicho, Dk John Magufuli na tingatinga na kuwa akiwa
Rais, Tanzania itanufaika sana.
Amesema Dk Magufuli akiwa Rais, kasi ya kusukuma maendeleo itakuwa kubwa sana na kuwa anamwamini na hataona haya kumwombea kura.
Rais Kikwete ameyasema hayo jana wakati akifunga Mkutano Mkuu Maalumu
wa CCM uliofanyika kwa siku mbili kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Dodoma
(DCC), Makulu mjini hapa.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulifanya uteuzi wa mgombea urais
wa CCM ambapo Dk Magufuli aliwashinda Balozi Amina Salum Ali na Dk
Asha-Rose Migiro kupewa dhamana hiyo.
Akimzungumzia Dk Magufuli, Rais Kikwete alisema waziri huyo wa Ujenzi
ni zaidi ya jembe, ni tingatinga kutokana na utendaji kazi uliotukuka.
“We bwana jembe, tena ni zaidi ya jembe, ndio maana nimesema wewe
tingatinga,” alieleza Rais Kikwete na kusema wajumbe wa mkutano huo
wamempa ushindi wa kishindo mgombea huyo.
Aliongeza, “Wamekupa imani kubwa, si imani ya kubahatisha, ni imani
uliyostahili. Ukiwa katika wizara mbalimbali ulithibitisha moyo wa
kupenda kuona kitu kinatendeka na msukumaji hasa wa mambo, umekuwa kama
bulldozer (tingatinga).”
Alisema Dk Magufuli alifanya hivyo katika Wizara ya Ardhi ambako wala
rushwa kwa kuuza viwanja walikiona cha moto, katika Uvuvi ambalo wavuvi
haramu hawakupona na katika Ujenzi, amesukuma sana ujenzi wa barabara
nchini.
Mbali ya kuwa Waziri wa Ujenzi kuanzia mwaka 2010 hadi sasa, Dk
Magufuli aliyezaliwa Oktoba 29, 1959 wilayani Chato, amewahi kuwa Waziri
wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, zote katika Serikali ya Rais Kikwete.
Katika Awamu ya Tatu, alikuwa Waziri wa Ujenzi kuanzia mwaka 2000
hadi 2005 na Naibu Waziri wa wizara hiyo kuanzia 1995 hadi 2000. “Kazi
yako haina mfano, wewe ni mfanyakazi hodari na mbunifu. Ukiwa Rais wa
nchi, Tanzania itanufaika sana na kasi ya kusukuma maendeleo itakuwa
kubwa sana.
“Ndugu Magufuli havumilii ujinga, mkandarasi wa ujenzi akikosea leo
kazi hana, injinia mbabaishaji hapo hapo atamfukuza. Watanzania mpate
nini tena?” Alihoji Rais Kikwete.
CHANZO HABARI LEO
Monday, 13 July 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


0 comments:
Post a Comment