Serikali imesema kuwa halmashauri zinazodaiwa na bodi ya Mikopo ya
Serikali za Mitaa na ambazo zimeshindwa kurejesha malimbikizo ya madeni
inayodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa hazitaruhusiwa kukopa
katika taasisi nyingine za kifedha hadi zikamilishe kwanza deni
llinalodaiwa na Bodi hiyo.
Agizo hilo limetolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe.George Simbachawene wakati alipotembelea
maonyesho ya wakulima ya nane nane yanayofanyika kitaifa mkoani Lindi.
Waziri Simbachawene alisema kuwa halmashauri zote zinazodaiwa na Bodi ya
Mikopo ya Serikali za Mitaa hataziruhusu kuomba mkopo wa fedha kutoka
taasisi nyingine zozote hadi kwanza zikamilishe deni walilokopa kutoka
katika Bodi hiyo.
Waziri Simbachawene alisema kuwa ameamua kufanya hivyo ili kuhakikisha
kuwa fedha zote zilizokopwa na halmashauri kwa ajili ya kutekeleza
miradi mbalimbali ya maendeleo zinarejeshwa ili mfuko huo uwe endelevu
na kuzipa fursa halmashauri nyingine kukopa fedha kutoka kwenye Bodi
hiyo.
Aidha Waziri Simbachawene ameitaka Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa
kuandaa utaratibu maalum utakaoziwezesha halmashauri zinazokopa fedha
kupitia taasisi hiyo zinarejesha fedha zake moja kwa moja benki bila ya
kukumbushwa mara kwa mara.
Hatua hiyo ya Waziri Simbachawene inafuatia maelezo ya Mhasibu wa Bodi
hiyo Bwana Mourice Kobalogira kumweleza Waziri kuwa Halmashauri nyingi
zilizokopa fedha kupitia Bodi hiyo zimekuwa zikikwepa kurejesha fedha
kwa visingizio mbalimbali hali inayosababisha chombo hicho kushindwa
kuzikopesha halmashauri nyingine.
Bwana Kobalogira alimweleza Waziri Simbachawene kuwa hali ya urejeshaji
mikopo imekuwa ya kusua sua mno ambapo hadi kufikia sasa maombi mapya ya
halmashauri zinazotaka kukopa kupitia bodi hiyo yamefikia bilioni 49
lakini Bodi imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni tisa
tu.
"Tatizo Mhe.Waziri ni kuwa halmashauri hazizingatii urejeshaji kulingana
na mikataba yao waliyoombea mikopo, mfano mtu kama aliomba mkopo kwa
ajili ya ujenzi wa kituo kikuu cha Mabasi, basi fedha za urejeshaji
zitoke katika mapato ya stendi, au kama halmashauri iliomba mkopo kwa
ajili ya ujenzi wa soko, fedha za urejeshaji zitokane na mradi huo,
lakini halmashauri nyingi zimekuwa hazifanyi hivyo," alisema bwana
Kobalogira.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Simbachawene aliiagiza Bodi hiyo kuhakikisha
kuwa inaweka kipengele katika mkataba wa mkopo utakaozibana halmashauri
hizo kurejesha fedha ilizoombea mkopo kulingana na masharti yaliyowekwa
na bodi hiyo, tofauti na ilivyo sasa ambavyo halmashauri nyingi
zilizopewa mkopo zimekuwa zikikwepa kutekeleza suala la marejesho.
tamisemi

0 comments:
Post a Comment