Sunday, 1 November 2015

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda.


BAADA ya kupatikana kwa Rais mteule wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli, anayetarajiwa kuapishwa Alhamisi ijayo, macho na masikio ya Watanzania, sasa yanaelekezwa kwa kiongozi wa mhimili wa Bunge, Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Tanzania imeongozwa na maspika watatu, Pius Msekwa, Samuel Sitta na Anne Makinda, ambao kisheria wanao uwezo wa kuomba kuteuliwa tena.
Ingawa sifa za kiongozi huyo, zimeainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tayari wachunguzi wa mambo wameelezea umuhimu wa Spika huyo kuwa na sifa za ziada, mbali na zilizoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumzia mtazamo wake kuhusu Spika ajaye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana alisema ni vyema atakayechaguliwa, awe mtu asiyeegemea chama chochote cha siasa bungeni.
“Kwa aina ya wabunge waliochaguliwa kwenye uchaguzi wa mwaka huu, utaona kuna mchanganyiko wa vijana na wageni wengi ambao ni mara ya kwanza bungeni, sasa ni vyema Spika atakayechaguliwa amsome rais wake, na aweze kwenda na kasi yake,” alisema Profesa Bana.
Alisema wabunge waliochaguliwa hivi sasa, pamoja na kwamba wapo baadhi waliokuwepo kwenye bunge lililopita, lakini uwepo wa vijana na wabunge wapya wengi, utaleta changamoto bungeni, kwani wananchi hivi sasa wamechagua wabunge wanaowaona ni wachapa kazi.
Kwa mujibu wa Profesa Bana, Dk John Magufuli ni mtu wa kazi na mwenye kupenda watendaji wachapakazi, hivyo ni vyema Spika ajaye awe na sifa ya ziada ya kumsoma rais na kwenda na kasi yake ili kuhakikisha nchi inasonga mbele.
“Tukimpata Spika atakayeliongoza Bunge vizuri kwa kasi, hasa ukizingatia wabunge waliochaguliwa wameona mwamko wa wananchi na kutambua wakilemaa tu wanapoteza nafasi hiyo.
“Nina hakika watajitahidi kutoa hoja zenye mashiko zaidi kwa ajili ya maslahi ya wananchi, hivyo Spika lazima awe na uwezo mzuri pia kichwani wa kutoa uamuzi kulingana na Kanuni za Bunge na busara pia,” alisema Profesa Bana.
Alisema Katiba ya Tanzania imeainisha sifa za Spika, ambapo kisheria anatakiwa kuchaguliwa na wabunge kutoka miongoni mwa watu ambao ni wabunge au wenye sifa za kuwa wabunge na sifa hizo zinaambatana na sifa za ziada, ili Bunge liongozwe vizuri na kuleta changamoto kwa Serikali.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 84(1) inafafanua kuwa “Kutakuwa na Spika wa Bunge ambaye atachaguliwa na wabunge kutoka miongoni mwa watu ambao ni wabunge au mwenye sifa za kuwa mbunge; atakuwa ndiye kiongozi wa Bunge na atawakilisha Bunge katika vyombo na vikao vingine vyote nje ya Bunge”.
Profesa Bana pia aliwataka wabunge wa vyama vyote, waliopata ridhaa ya wananchi kwenye majimbo yao, kuondoa tofauti zao, kwani uchaguzi umekwisha na sasa waungane kuwa timu moja, itayakofanya kazi ya kujenga nchi badala ya kuendelea kulalamika.
Aliwashauri wabunge hao waendapo bungeni, wajiepushe na tabia ya ubinafsi ya kudai maslahi yao, kama ilivyoonekana kwenye Bunge la 10, na badala yake waweke maslahi ya nchi mbele.
Jaji Mutungi Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema pamoja na sifa za kwenye Katiba, ni vyema Spika ajaye awe mtu mwenye maadili ya kazi. “Spika ni mtu yeyote mwenye sifa zilizoainishwa kwenye Katiba, lakini pia awe na sifa za ziada ambazo ni pamoja na kuzingatia maadili ya kazi yake na maslahi ya nchi,” alisema Jaji Mutungi.
Aliongeza kuwa ni vyema wabunge watumie busara, kumchagua mtu mwenye hekima na busara, atakayeweza kuwaongoza na kutoa maamuzi yanayoleta tija kwa maslahi ya Taifa kwanza.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 84(2) inaeleza kuwa “Waziri, naibu waziri au mtu mwenye madaraka ya aina nyingine yoyote, itakayotajwa na sheria iliyotungwa na Bunge kwa madhumuni ya ibara hii, hataweza kuchaguliwa kuwa Spika.chanzo habari leo

0 comments:

Post a Comment

wanaotutazama


hit counter

tz shiling exchange

MY CALENDAR

Total Pageviews

Recent Posts

find us on twitter

Find Us On Facebook

MATANGAZO