SERIKALI imesema ipo katika hatua za mwisho kuanzisha maduka ya dawa katika hospitali zake zisizokuwa nayo na kuweka maduka mapya ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD), hatua itakayohakikisha dawa zinapatikana katika hospitali hizo.
Aidha, imesema ili kufanikisha hilo, inafanya mazungumzo na wamiliki binafsi wa maduka ya dawa yaliyo nje ya hospitali zote za serikali ili yahamishwe kuondoa mgongano wa kimaslahi baada ya kubaini maduka mengi ni ya watumishi wa afya.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando, aliyasema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road na kufafanua zaidi kwa simu alipozungumza na gazeti hili baada ya ziara hiyo.
Dk Mmbando alisema changamoto ya dawa ipo katika maeneo mengi ya nchi, hivyo serikali imeandaa utaratibu wa kuweka maduka ya dawa ya serikali ndani ya hospitali zake ambayo yatasaidia upatikanaji wa dawa kwa wepesi na kwa bei rahisi. “Maduka ya dawa hayapo katika hospitali zote.
Tuliruhusu kuwepo kwa maduka binafsi ili kuongeza ushindani wa dawa, lakini baadhi ya watumishi wasio waaminifu wanawaandikia wagonjwa dawa wanazojua katika duka la hospitali hakuna, na kumwagiza aende duka la nje ambalo ni lake ama la mwenzake.
“Mpango tunaouzungumza hapa ni kuweka maduka katika hospitali za serikali zisizo nayo na pia kuanzisha maduka ya MSD ndani ya hospitali moja kwa moja ili kuhakikisha dawa stahiki zote zinapatikana kwa wakati,” alifafanua Dk Mmbando.
Alisema hatua hiyo itaondoa ucheleweshwaji wa kupata dawa kwa wakati na itaongeza ufanisi. Kadhalika alisema hivi sasa utekelezaji wa mpango huo unaendelea hatua kwa hatua. “Hilo suala limezungumzwa vizuri pia katika bajeti tunayoitekeleza katika mwaka huu wa fedha (2015/2016) na tutaeleza utekelezaji wake mwakani,” alisema Dk Mmbando.
“Wananchi wamekuwa wakilalamika kukosa dawa ndani ya hospitali na kutakiwa kununua katika maduka ya nje, jambo ambalo limeleta sintofahamu kwa wananchi, hivyo kwa sababu maduka yote ya dawa yamesajiliwa kisheria tunataka kuyaondoa kwa maana ya kuyahamisha ili kuondoa huo mgongano,” alibainisha Dk Mmbando.
Katika hatua nyingine, Serikali imezitaka hospitali zake zote nchini kuhakikisha zinatenga bajeti itakayowasaidia kufanya marekebisho ya vifaa tiba pindi vitakapoharibika ili kuondoa usumbufu kwa wagonjwa.
Dk Mmbando alisema hospitali hizo zinapaswa kuweka bajeti ya vifaa tiba itakayowasaidia wao kama hospitali kufanya marekebisho na kuacha kusubiri mpaka serikali itoe fedha za marekebisho ya vifaa hivyo.
“Hospitali hizi tunajua zinapata fedha, hatutegemei kusikia malalamiko ya vifaa kuharibika, lazima wachukue hatua wao wenyewe za kuhakikisha vifaa vinarekebishwa ili kuondoa usumbufu kwa wagonjwa na kuwanyima haki ya msingi ya kupatiwa huduma bora,” alisema Katibu Mkuu huyo. chanzo habari leo

0 comments:
Post a Comment