Friday, 16 October 2015

Rais Jakaya Kikwete akimwaga udongo kwenye kaburi la Dk Abdallah Kigoda
RAIS Jakaya Kikwete ameongoza mamia ya waombolezaji katika maziko ya aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda yaliyofanyika nyumbani kwake Chanika wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Maziko yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo Spika Anne Makinda, Jaji Mkuu Othmani Chande, Mufti Shekhe Abubakari Zuberi, mawaziri, manaibu, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya, wawakilishi wa wenye viwanda na wafanyabiashara, viongozi wa kisiasa na wawakilishi mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alisema Taifa limempoteza mtaalamu makini wa mipango ambaye alikuwa na mlengo wa kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kwa kuwekeza kwenye viwanda hatua ambayo ililenga kuleta maendeleo ya haraka.
Naye Spika wa Bunge, Makinda alimzungumzia Dk Kigoda kama kiongozi mnyenyekevu aliyethamini maendeleo ya Watanzania mshauri mkuu wa masuala ya uchumi ndani ya Bunge.
Kwa upande wake, Mwakilishi vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar, Salum Mwalimu alisema Dk Kigoda amekuwa kielelezo kizuri na mfano wa kuigwa kwa wanasiasa vijana.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya wabunge wa mkoa wa Tanga, Mbunge wa Jimbo la Mlalo anayemaliza muda wake, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi alisema Dk Kigoda alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge wa Mkoa wa Tanga na kwamba katika kipindi chote hicho aliwaongoza vizuri. Naye mwakilishi wa waumini wa dini ya Kikristo, Askofu John Mwakyusa alisema daima marehemu atakumbukwa kutokana na mema yake bila kujali itikadi za kidini.
Akitoa wasifu wa marehemu, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Uledi Mussa alisema Dk Kigoda alikuwa ni mtaalamu aliyebobea katika masuala ya uchumi ambapo alifanikiwa kushika nyadhfa mbalimbali za uongozi kama mtaalamu wa uchumi kwenye wizara mbalimbali.
Jana asubuhi jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal aliongoza waombolezaji kumuaga Dk Kigoda aliyefariki dunia Jumatatu wiki hii kwenye Hospitali ya Apollo, New Delhi, India alikolazwa kwa matibabu.
Spika Makinda alisema, “ni mbunge wa 12 kufariki katika Bunge la 10 na wa nne kufa tangu Bunge lilipovunjwa…alikuwa makini katika utendaji wake. Hakuonekana mdhaifu, lakini sasa amefariki.”
Dk Kigoda aliyezaliwa Novemba 25, 1953 katika kijiji cha Lwengera wilayani Korogwe, alikuwa Mbunge wa Handeni kwa miaka 20, na alikuwa mgombea ubunge wa CCM katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu.
Msomi huyo aliyeacha mjane, watoto wanne na wajukuu wanne, aliongoza wizara za Nishati na Madini, Mipango na Ubinafsishaji, Viwanda na Biashara pamoja na kufanya kazi katika Tume ya Mipango kama mchumi na Ofisi ya Waziri Mkuu kama mchumi. chanzo habari leo

0 comments:

Post a Comment

wanaotutazama


hit counter

tz shiling exchange

MY CALENDAR

Total Pageviews

Recent Posts

find us on twitter

Find Us On Facebook

MATANGAZO