Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015 tulieleza malengo yetu kwa wananchi. Tunawakumbusha malengo hayo. Tutakuwa tunatoa mrejesho wa utekelezaji kila wakati. Siku ya Jumanne tarehe 9/8/2016 tutatoa mrejesho wa kwanza.
Tunataka kuwaonyesha watanzania kuwa ACT Wazalendo ikipewa dhamana inatimiza. Kwamba Siasa za sasa ni Siasa za Maendeleo ( developmental politics ) na sio Siasa za porojo. Tuliahidi kutumia Manispaa ya Kigoma kama mfano wa namna tungeendesha Nchi yetu.
Haya hapa chini ndio malengo yetu kama tulivyowaeleza wananchi wakati wa kampeni.
1. Kushirikiana na Wabunge wa Mkoa wa Kigoma kuhakikisha barabara zote za mkoa zinaunganishwa Kwa Lami. Barabara za Kigoma - Nyakanazi, Mwandiga - Kagunga na Simbo - Kalya ni mfano wa barabara hizo.
2. Kuhakikisha kuwa Mitaa ya Manispaa inakuwa na miradi maalumu ya kujengwa mifereji na barabara za Lami na mawe Kwa lengo la kusafisha mji na kuzalisha ajira Kwa vijana. Pia kumaliza kero za miundombinu Mto Luiche kata ya Kagera [ kwa kujenga daraja na barabara kutokea Ujiji ].
3. Kuboresha mazingira ya Biashara Kwa kuondoa kero ya ushuru Kwa wafanyabiashara wadogo Kwa mujibu wa Sheria ndogo za Manispaa, kuboresha Bandari zote na kujenga bandari mpya(jetty) eneo la Forodha ya Ujiji ili kurudisha hadhi ya mji wa Ujiji.
4. Kuhamasisha vikundi vya Wananchi kama wavuvi, kina mama, wakulima wa bustani, waendesha vyombo vya usafiri na kuviunganisha na mifuko ya hifadhi ya jamii Kwa kuchangia sehemu ya michango yao ili wapate mafao ya kama mikopo nafuu na Bima ya afya. 50% ya Bajeti ya Mfuko wa Mbunge itachangia Mfumo wa Hifadhi ya Jamii wa Manispaa.
5. Kushirikiana na Wabunge wa Mkoa wa Kigoma kuanzisha Benki ya Kigoma ili kuwezesha Wafanyabiashara wa Kigoma kukuza mitaji yao na hivyo kupanua [ Biashara ] zao.
6. Kusimamia kikamilifu kuanza Kwa Mradi wa kufua umeme Kwa kutumia maporomoko ya maji katika Mto Malagarasi ( Igamba III ) na kumaliza kabisa tatizo la umeme wa uhakika mkoani Kigoma.
7. Kuhakikisha Mradi mkubwa wa Mpunga katika Bonde la Mto Luiche unaanza ili kuzalisha ajira katika Kilimo na Viwanda vya Mazao ya kilimo.
8. Kumaliza tatizo la fidia Kwa waliopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma [ Gombe-Mahale International Airport ] na miradi ya Bandari Kavu Kibirizi na Katosho
9. Kusimamia uanzishwaji wa Viwanda kupitia KiSEZ. Tutaanza na Viwanda vya mazao ya Mawese/Michikichi na viwanda vya kuchakata Samaki kufuatia kuboresha Uvuvi.
10. Kuendelea kuwatetea watu wa Kigoma dhidi ya unyanyasaji kuhusu uraia wao na kukomesha kabisa manyanyaso hayo Kwa kuhakikisha kuwa kipaombele cha vitambulisho vya uraia kinakuwa mji wa Kigoma.
11. Kuanzisha timu ya soka ya manispaa na kuhakikisha inafika ligi kuu.Hii litaenda na kuanzidhwa Kwa shule Maalumu ya Michezo (sports academy) ili kukuza vipaji vya Soka.
12. Kukuza Utalii ili kuzalisha ajira Kwa vijana wengi zaidi wa mkoa wa Kigoma.
13. Kufuatilia kikamilifu na kumaliza kabisa changamoto ya wavuvi kuvamiwa na kuporwa Mali zao
14. Kukamilisha mradi mkubwa wa Maji ili kumaliza tatizo la maji; kupitia Hifadhi ya Jamii kuhakikisha kila mwananchi anapata matibabu; na kusimamia kikamilifu uboreshwaji wa elimu katika manispaa - kuboresha Chuo cha VETA, Kuanzisha High School 2 na kuboresha Shule za Msingi.
15. Kuanzisha na kuendesha Jukwaa la viongozi wa Dini ili kuendeleza mahusiano mema Kati ya waumini wa dini mbalimbali.
Tarehe 9/8/2016 tutatoa mrejesho wa nini tumeshafanya mpaka sasa ikiwemo ' bonus ' kadhaa, yaani tuliyoyafanya ziada ya ahadi tulizotoa tangu tumechaguliwa kuunda Baraza la Madiwani la Manispaa ya Kigoma Ujiji
Zitto Ruyagwa Zuberi Kabwe, Mb
Kigoma - Ujiji.

0 comments:
Post a Comment